Kiongozi wa Democratic nchini Marekani kujiuzulu

Debbie Wasserman Schultz
Kiongozi wa Chama cha Democratic nchini Marekani amesema atajiuzulu baada ya barua pepe zilizofichuliwa na kuchapishwa na mtandao wa WikiLeaks kudokeza huenda maafisa wakuu wa chama walijaribu kuvuruga kampeni ya Bernie Sanders.
Ufichuzi huo umetishia kuvuruga umoja katika chama hicho.
Seneta wa Vermont Bernie Sanders, alikuwa amemshinikiza Debbie Wasserman Schultz, mwenyekiti wa Kamati Kuu ya Kitaifa ya chama cha Democratic, ajiuzulu mkesha wa kufanyika kwa kongamano.
Bi Hillary Clinton, aliyekuwa akishindana na Bw Sanders katika kutafuta tiketi ya chama cha Democratic, anatarajiwa kuidhinishwa rasmi kuwa mgombea katika kongamano kuu la chama mji wa Philadelphia.
Bw Sanders alisema Bi Wasserman Schultz "hafai kuwa mwenyekiti” wa Kamati Kuu ya Kitaifa ya chama cha Democratic.
"Na nafikiri barua pepe hizi zinatilia mkazo msimamo wetu kwamba hafai kuwa mwenyekiti,” ameambia kipindi cha This Week cha runinga ya ABC.
Kwa muda mrefu kambi ya Bw Sanders imekuwa ikimtuhumu Bi Wassermann Schultz na wakuu wengine wa chama kwa kumpendelea Bi Clinton.
Barua pepe karibu 19,000 zilizochapishwa kwenye mtandao wa WikiLeaks mnamo 22 Julai ni za viongozi saba wakuu wa kamati kuu ya chama cha Democratic.
Baadhi zinaonesha baadhi ya maafisa walijaribu kutumia mbinu nyingi ikiwemo suala la imani kuvuruga kampeni ya Bw Sanders.
Debbie Wasserman Schultz
Bi Wassermann Schultz anatarajiwa kujiuzulu baada ya kumalizika kwa kongamano la kuidhinisha mgombea. Anatarajiwa kufungua na kufunga kongamano, na pia atahutubu.
Rais Barack Obama amemshukuru kwa mchango wake kwa chama.
Hayo yakijiri, Bw Sanders na wafuasi wake pia wameeleza kusikitishwa kwao na hatua ya Bi Clinton kumteua Seneta wa Virginia Tim Kaine kuwa mgombea mwenza wake.
Badala yake, walitaka mtu anayeegemea zaidi siasa za mrengo wa kushoto.
Hata hivyo, Bw Sanders alisema: “Nimemfahamu Tim Kaime kwa miaka kadha … Tim, ni mtu mwerevu, mwerevu sana. Ni mtu mzuri.”
Bi Clinton alipigwa jeki Jumapili baada ya meya wa zamaniwa New York, aliyechaguliwa kupitia chama cha Republican, Michael Bloomberg, kumuunga mkono.
Kongamano la chama cha Democratic litaanza Jumatatu kwa hotuba za Mke wa Rais Michelle Obama na Bw Sanders.
Kongamano hilo litaendelea kwa siku nne, na limeandaliwa baada ya kongamano la chama cha Republican kumuidhinisha Donald Trump wiki iliyopita.
Kiongozi wa Democratic nchini Marekani kujiuzulu Kiongozi wa Democratic nchini Marekani kujiuzulu Reviewed by Ino on 11:13:00 PM Rating: 5

No comments:

ino mo. Powered by Blogger.