Libya yajiondoa kuandaa AFCON2017

Libya imekiri usalama umedorora
Libya imejiondoa kuwa mwenyeji wa mashindano
ya kuwania kuwa mabingwa wa Afrika mwaka wa 2017.Ujumbe wa taifa hilo lililogubikwa na vita limesema kuwa vita vinavyoendelea nchini humo vimewanyima fursa ya kujenga viwanja na makao ya timu zitakazoshiriki mashindano hayo.
Kufuatia kauli hiyo shirikisho la soka barani Afrika CAF sasa limeomba mataifa badala kutuma maombi ya kutaka kuwa wenyeji wa mashindano hayo yanayohusisha timu 16.
Mataifa yanayotaka kuandaa mashindano hayo yana muda wa hadi septemba tarehe 30 kutuma maombi yao.
Caf itatangaza mwenyeji mpya wa mashindano hayo mwakani.
Shirikisho la CAF linasema kuwa linatafuta taifa lenye uwezo wa kuhakikishia washiriki makao usalama viwanja na muundo msingi bora wa usafiri wao .

Mapigano baina ya makundi tofauti yamesababisha mashindano kuahirishwa.
Libya ilikuwa imeahidi kujenga viwanja 11 kwa gharama ya dola milioni 314 za Marekani ikiwemo uwanja wenye viti 60,000 uliokuwa unastahili kujengwa katika kambi ya zamani ya jeshi mjini Tripoli.
Miji ya Benghazi na Misrata ilikuwa imeratibiwa kujengewa viwanja vipya lakini miji hiyo ndiyo iliyokuwa chimbuko la vita vilivyomng'oa mamalakani Gaddafi.
Tayari ligi kuu ya Libya imeahirishwa kwa hofu ya kuwa timu shiriki zitashindwa kuhakikishia usalama wao.

Mataifa yenye uwezo wa kuandaa makala ya 2017 ya AFCON yana mwezi mmoja kutuma maombi yao
Sadfa ni kuwa kwa mara ya kwanza Libya ndiyo iliyotawazwa mabingwa wa kombe la Afrika kwa wachezaji wa ligi za nyumbani yaani CHAN .
Vilevile Caf inatarajiwa kutangaza mwenyeji wa makala ya mwaka wa 2019 na 2021 katika mkutano wake mkuu utakaoandaliwa mjini Addis Ababa Ethiopia 20 Septemba.
Algeria, Cameroon, Guinea, Ivory Coast na Zambia zimetangaza azimio la kuandaa mashindano hayo
Libya yajiondoa kuandaa AFCON2017
Reviewed by Ino
on
10:02:00 PM
Rating:
No comments:
Post a Comment